Saturday, 5 November 2016

Upimaji afya kwa waliokuwa wafanyakazi wa bulyanhulu waendelea

Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) unaendesha zoezi maalum la upimaji afya za waliokuwa wafanyakazi wa mgodi wa Bulyanhulu ambao waliachishwa kazi na mgodi huo mnamo mwaka 2007 bila kupimwa afya zao kinyume na Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.
Mpango huo ulibainishwa na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Dkt. Akwilina Kayumba, alipozungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam juzi. Dkt. Kayumba alieleza kwamba zaidi ya wafanyakazi 90 wataonwa na madaktari bingwa wa hospitali ya Taifa ya Mhimbili na hospitali ya rufaa ya Bugando.
“Baada ya ukikwaji huo wa sheria kuripotiwa kwa Wakala mwaka 2013, hatua stahiki zilichukuliwa ikiwemo kufanya kaguzi maalum  za usalama na afya katika eneo la mgodi na kutoa onyo kali kwa mwajiri wa walalamikaji ikiwa ni pamoja na kumtaka kugharimia upimaji afya za waathirika wote,” alisema Mtendaji Mkuu.
Aliongeza kuwa: “Katika kushughulikia tatizo hilo, vikao vya mashauriano vilivyojumuisha serikali, mwajiri (Mgodi wa Bulyanhulu) na waathirika kupitia chama chao, TAMICO, vilifanyika na utaratibu wa kushughulikia suala hilo ukawekwa.”
Alisema katika utaratibu huo, TAMICO ilipewa jukumu la kuwatafuta waathirika wote popote walipo na kuwasilisha majina yao kwa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi. Wakala ulikuwa na jukumu la kuyapeleka majina hayo kwa mwajiri kwaajili ya uhakiki na kuratibu upimaji afya wa waathirika hao baada ya majina yao kuhakikiwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wakala iliyotolewa kwa vyombo vya habari, hadi kufikia sasa tayari waathirika 315 kati ya 371 ambao mwajiri alithibitisha kwamba walikuwa wafanyakazi wake wameshapimwa afya zao. Waathirika 56 waliobaki hawakujitokeza wakati wa upimaji afya licha ya kupewa taarifa juu ya zoezi hilo. 
“Waathirika watakaopimwa kwasasa ni wale ambao vipimo vyao vya awali vilionesha kwamba wanahitaji vipimo zaidi kutoka kwa madaktari bingwa”.
Aidha taarifa hiyo ilifafanua kwamba maandalizi ya upimaji huo yamekamilika na zoezi hili litafanyika katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili siku ya Jumamosi tarehe 20/08/2016 na katika hospitali ya rufaa ya Bugando mnamo tarehe 22/08-15/09/2016.

No comments:

Post a Comment

Note: only a member of this blog may post a comment.